Joel 1

1 aNeno la Bwana ambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli.

Uvamizi Wa Nzige


2 bSikilizeni hili, enyi wazee;
sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi.
Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea
katika siku zenu au katika siku za babu zenu?

3 cWaelezeni watoto wenu,
na watoto wenu wawaambie watoto wao,
na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata.

4 dKilichosazwa na kundi la tunutu
nzige wakubwa wamekula,
kilichosazwa na nzige wakubwa
parare wamekula,
kilichosazwa na parare
madumadu wamekula.

5 eAmkeni, enyi walevi, mlie!
Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo,
pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya,
kwa kuwa mmenyang’anywa
kutoka midomoni mwenu.

6 fTaifa limevamia nchi yangu,
lenye nguvu tena lisilo na idadi;
lina meno ya simba,
magego ya simba jike.

7 gLimeharibu mizabibu yangu
na kuangamiza mitini yangu.
Limebambua magome yake
na kuyatupilia mbali,
likayaacha matawi yake yakiwa meupe.


8 hOmboleza kama bikira aliyevaa nguo ya gunia
anayehuzunika kwa ajili ya mume wa ujana wake.

9 iSadaka za nafaka na sadaka za kinywaji
zimekatiliwa mbali kutoka nyumba ya Bwana.
Makuhani wanaomboleza,
wale wanaohudumu mbele za Bwana.

10 jMashamba yameharibiwa,
ardhi imekauka;
nafaka imeharibiwa,
mvinyo mpya umekauka,
mafuta yamekoma.

11 kKateni tamaa, enyi wakulima,
lieni, enyi mlimao mizabibu;
huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri,
kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa.

12 lMzabibu umekauka
na mtini umenyauka;
mkomamanga, mtende na mtofaa,
miti yote shambani, imekauka.
Hakika furaha yote ya mwanadamu
imeondoka.

Wito Wa Toba


13 mVaeni nguo ya gunia, enyi makuhani, muomboleze;
pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni.
Njooni, vaeni nguo ya gunia usiku kucha,
enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu;
kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji
zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu.

14 nTangazeni saumu takatifu;
liiteni kusanyiko takatifu.
Iteni wazee
na wote waishio katika nchi
waende katika nyumba ya Bwana Mwenyezi Mungu wenu,
wakamlilie Bwana.


15 oOle kwa siku hiyo!
Kwa kuwa siku ya Bwana iko karibu;
itakuja kama uharibifu
kutoka kwa Mwenyezi
Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania.


16 Je, chakula hakikukatiliwa mbali
mbele ya macho yetu:
furaha na shangwe
kutoka nyumba ya Mungu wetu?

17 Mbegu zinakauka
chini ya mabonge ya udongo.
Ghala zimeachwa katika uharibifu,
ghala za nafaka zimebomolewa,
kwa maana hakuna nafaka.

18 Jinsi gani ng’ombe wanavyolia!
Makundi ya mifugo yanahangaika
kwa sababu hawana malisho;
hata makundi ya kondoo yanateseka.


19 Kwako, Ee Bwana, naita,
kwa kuwa moto umeteketeza
malisho ya mbugani
na miali ya moto imeunguza
miti yote shambani.

20 Hata wanyama wa porini wanakuonea shauku;
vijito vya maji vimekauka,
na moto umeteketeza
malisho yote ya mbugani.
Copyright information for SwhKC